Thursday, 29 December 2016

Kama unatabia hizi 10 basi tayari wewe ni Mjasiriamali.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala mkubwa ikiwa mjasiriamali anazaliwa au anatengenezwa. Kwa kuangalia tabia za wajasiriamali na tabia za binadamu kwa ujumla, wajasiriamali wana tabia za kipekee. Wajasiriamali wanafikiri tofauti na wanatenda tofauti na watu wengine kwenye jamii.

Tabia za kipekee zinazooneshwa na wajasiriamali kuna ambao wamezaliwa nazo na kuna ambao wamezipata kutoka kwenye mazingira na shughuli wanazofanya.

Hapa nitaelezea tabia 10 ambazo ni dalili tosha kwamba wewe ni mjasiriamali. Kama huna tabia hizi unaweza ukaanza kujifunza taratibu na baadae ukawa na tabia za kijasiriamali. Kumbuka tofauti kubwa ya mjasiriamali ni jinsi anavyofikiri na kuchukua hatua tofauti na watu wengine. Kwa mfano wakati mwajiriwa anaweza kukubaliana na shida anazopata kwenye ajira yake na kuona hakuna anachoweza kufanya, mjasiriamali anafikiria uwezo wa tofauti alionao na jinsi anavyoweza kwenda kuutumia nje ya ajira na akafanikiwa. Baada ya hapo anaweza kuacha kazi na kwenda kufanya lile litakalomridhisha. Kwa kuwa na mtizamo chanya na utayari wa kuchukua hatua kunawafanya wajasiriamali kupata mafanikio makubwa.

Kama unatabia hizi 10, ni dalili tosha kwamba wewe ni mjasiriamali, unatakiwa kuchukua hatua mara moja ili kufikia mafanikio makubwa;

1. Hukubaliani na mfumo. Mara nyingi umekuwa ukihoji kwa nini kitu fulani kifanyike na umekuwa ukijitahidi kutafuta njia bora zaidi ya kufanya kazi fulani pale unapokuwa umeajiriwa. Hufanyi kitu bila ya kuhoji umuhimu wake na kufikiri njia ya kuboresha.

2. Unaonekana kama mfanyakazi mkorofi. Wakati mwingine umeshafukuzwa kazi mara kadhaa kutokana na tabia yako ya kuhoji na kutaka kuboresha utendaji kazi. Au umeshaacha kazi au kupanga kufanya hivyo kutokana na kutoridhishwa na kazi hiyo.

3. Una hamasa kubwa ya kutekeleza majukumu yako. Husubiri upangiwe cha kufanya, unajua majukumu yako na unayafanya kwa ubora wa hali ya juu.

4. Ukiambiwa hapana huridhiki, hapana sio jibu kwako unaendelea kutafuta njia nyingine mpaka upate NDIYO.

5. Unajiamini na unaamini una uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa. Una uhakika hata kitokee kitu gani bado unauwezo wa kusimama na kuleta tofauti.

6. Ni mtu wa watu, unaweza kuchangamana na watu wa aina zote. Huna ubaguzi wa aina gani ya watu unaweza kukaa nao, popote unapokutana na watu unaweza kuanzisha mazungumzo na mkaenda vizuri.

7. Huogopi sana juu ya usalama wa ajira kwani unaamini hata bila ya ajira bado unaweza kuendesha maisha yako.

8. Mara kadhaa umekuwa ukigomea mamlaka. Umekuwa ukikataa maelekezo yanayotolewa na mamlaka kama hayaendani na misimamo yako ya ufanyaji kazi bora. Hii imekupelekea kuonekana ni mfanyakazi mkorofi na hata kufukuzwa.

9. Siku za mapumziko kama sikukuu au mwisho wa wiki ndio siku bora kwako kufanya kazi zako binafsi, huendekezi kupoteza muda kwa kupumzika au kustarehe.

10. Umewahi kuuza vitu vidogo vidogo ulipokuwa mtoto. Pia umewahi kufuga kuku, sungura na hata njiwa enzi za utotini.


No comments:

Post a Comment