Wednesday, 28 December 2016

Wezi wa meno ya Tembo ya sh.300 milioni wafungwa miaka 15

Morogoro. Mahakama ya Wilaya ya Morogoro imewahukumu watu watatu kifungo cha miaka 15 jela kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kupatikana na vipande 51 vya meno ya tembo vyenye thamani ya zaidi ya Sh300 milioni.

 Baada ya hukumu kusomwa wake na ndugu wa washtakiwa wameangua vilio hali iliyowafanya askari kuwaondoa na kuwapeleka nje ya jengo la Mahakama ili kuruhusu shughuli zingine kuendelea.

 Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Joyce Mkoi dhidi ya washtakiwa Abel Adrian na Anael Mkindi, wakazi wa Dar es Salaam na Erick Kyaruzi, mkazi wa Shinyanga.

 Mkoi amesema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashtaka ambao haukuacha shaka yoyote kwamba washtakiwa walitenda kosa hilo.

 Amesema biashara ya meno ya tembo inasababisha wanyama hao kuuawa hivyo kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na utalii.

Kabla ya adhabu hiyo kutolewa, washtakiwa kwa nyakati tofauti waliiomba Mahakama iwapunguzie adhabu wakidai wana familia zinazowategemea.

 

Kyaruzi amedai mke wake ana umri mdogo na hilo ni kosa lake la kwanza. Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Costantine Kakula uliiomba Mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya washtakiwa kwa madai kuwa vitendo vya ujangili vimekithiri.

Washtakiwa walitenda kosa hilo Februari 8, 2012 eneo la Maseyu, Barabara ya Morogoro – Dar es Salaam.

 Ilidaiwa mahakamani kuwa idadi hiyo ya vipande vya meno hayo ni sawa na tembo 11 waliouawa.

 Ilidaiwa washtakiwa walikamatwa wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser lililobadilishwa namba ya usajili.

Upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi tisa katika kesi hiyo ambayo washtakiwa walijitetea wenyewe.

No comments:

Post a Comment